Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, wakati vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikiendelea siku hizi kwa lengo la kuilazimisha Tehran kutoa marupurupu na kujisalimisha bila masharti yoyote, kundi la wasomi na watu mashuhuri wa kisiasa, wanahabari na wanaharakati wa utamaduni nchini Iraq limewataka wananchi na serikali ya nchi yao kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutumia uwezo na nyenzo zote walizonazo. Wamesisitiza kuwa uungaji mkono huo ni wajibu wa kidini, kimaadili na kibinadamu ambao hauwezi kukwepeka kwa hali au mazingira yoyote yale.
Wairaqi wanasisitiza kuwa; ni lazima kuwe na msimamo ulio wazi, wa bayana na wa kishujaa dhidi ya kila uchokozi mpya wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu mahusiano na uhusiano wa kihistoria, kiitikadi, kijamii na kidini unaoziunganisha nchi hizi mbili jirani, pamoja na changamoto za pamoja za kiusalama na kisiasa, vinaitaka Iraq isikae kimya wakati inapoona nchi jirani inakabiliwa na hatari na uchokozi kutoka kwa maadui wa dini na ubinadamu, pamoja na vinara wa vita vya uchokozi na uharibifu walioko Washington na Tel Aviv.
Msimamo wa wazi wa Wairaqi
Abbas al-Miryani, mwandishi na mwanaharakati wa masuala ya habari, amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi jirani na ndugu yetu, na misimamo yake kuhusiana na Iraq daima imekuwa ya heshima na yenye kutukuka; iwe katika miaka ya vikwazo vya kiuchumi au baada ya kuangushwa kwa utawala wa Baath wa Saddam, na hasa katika kipindi cha vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh. Hakuna nchi yoyote ya Kiarabu jirani au ndugu iliyochukua misimamo kama hiyo.
Kwa hiyo, si jambo la kimantiki wala la kimaadili kwa viongozi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi nchini Iraq kujibu misimamo hiyo ya Iran kwa kujisalimisha na kunyamaza mbele ya mashambulizi ya Marekani na Israel, wakati ambapo Iraq inageuzwa kuwa njia ya kupitisha mashambulizi hayo au eneo la kuanzia kwa uchokozi huo wenye kuangamiza.
Baghdad Hairuhusiwi Kugeuza Ardhi na Anga Yake kuwa Jukwaa la Kuishambulia Iran
Al-Miryani amesisitiza kuwa; msimamo wa serikali ya Iraq unapaswa kuwa wazi na kusikika bayana. Amesema Iraq inapaswa kutoruhusu nchi zinazofanya uchokozi kukiuka anga yake au kuingia katika ardhi yake, wala kuifanya ardhi au anga hiyo kuwa sehemu ya kuanzia mashambulizi dhidi ya Iran. Ameeleza kuwa hilo ndilo jambo pekee ambalo Iran inalitaka, na haitaki jambo jingine lolote.
Ameongeza kuwa kosa lolote katika tathmini na mahesabu ya serikali ya Iraq kuhusu mgogoro unaotarajiwa linaweza kuisababisha Iraq kuwa sehemu ya mapambano hayo. Hili ni jambo ambalo hakuna mtu mwenye busara anayelitaka, hasa ikizingatiwa kuwa Israel inatamani sana kuona kosa la aina hiyo likitokea.
Kwa msingi huo, uamuzi wa Iraq unapaswa kuwa wa pamoja na kuzingatia uhuru na mamlaka yake ya kujitawala, mbali na mashinikizo na maagizo kutoka nje. Aidha, Iraq inapaswa kuwa mshiriki hai katika juhudi za kuleta utulivu katika eneo hili, kwa kushirikiana na ndugu na majirani zake.
Maoni yako